Friday, 7 June 2013

Watoto watukutu wakipewa mafunzo wanabadilika na kuwa wema.

Na Anna Nkinda – Singapore.
Watoto waliotengwa na jamii kutokana na tabia ya kutokuwa na maadili mazuri  (watukutu)  kama watapewa nafasi ya kupata mafunzo  ya kutosha ya dini, elimu ya darasani  na kuonyeshwa msingi mzuri wa maisha wanaweza kubadilika na kuwa watoto wema.
Hayo yamesemwa leo na Mama Sahnim Sokaimi ambaye ni mkuu wa kituo cha kurekebisha tabia za watoto wa kike watukutu cha PERTAPIS kilichoko nchini Singapore wakati akiongea na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipotembelea kituo hicho.
Alisema kuwa chuo hicho kinawapokea watoto wa kike kuanzia umri wa miaka 12 hadi 21 ambao mahakama imewakuta na makosa mbalimbali ikiwa  ni pamoja na uvutaji wa sigara chini ya miaka 18, utumiaji wa madawa ya kulevya na kufanya biashara ya kuuza mwili (sexual activities).
“Tuliamua kuanzisha kituo hiki baada ya kuona kuwa kuna tatizo kubwa la kuharibikiwa kwa watoto ikiwa ni pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya lakini baada ya watoto hawa kuwapa misingi mizuri ya malezi na maisha wameweza kubadilika na kuwa wasichana  wema wanaofuata dini”, alisema Mama Sokaimi.
Aliendelea kusema kuwa wasichana hao wamehukumiwa na mahakama kifungo cha miezi sita hadi miaka mitatu kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya na wakiwa katika kituo hicho wanapata mafunzo ambapo baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya makosa yao wanakuwa wamebadilika kitabia na kurudi kulelewa na familia zao.  
Alimalizia kwa kusema kuwa wazazi wanatakiwa kuchangia gharama za watoto wao kupata mafunzo kituoni hapo kiasi cha dola za Singapore 250  lakini wazazi wengi hawafanyi hivyo jambo ambalo linasababisha kituo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha na hivyo kuomba msaada kutoka kwa wadau mbalimbali.
Kwa upande wake mama Kikwete aliwapongeza wafanyakazi wa kituo hicho kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kurekebisha tabia za watoto wa kike ambazo hazikubaliki na jamii na kuwafanya kuwa wasichana na wamama wazuri ambao wanafanya kazi mbalimbali za kujitegemea kimaisha.
Mama Kikwete alisema kuwa  jukumu la kuwalea na kurekebisha tabia za watoto ni la jamii nzima na kuwaomba wafanyakazi wa kituo hicho kuja  nchini ili nao wajifunze na kuona ni jinsi gani wanaweza kushirikiana  kwa pamoja kuwasaidia watoto wenye matatizo kama hayo.
Aidha mama Kikwete pia alitumia taaluma yake ya ualimu na kutumia muda mfupi aliokutana na wasichana hao na kuwafundisha somo la kiingereza kwa kuwaelekeza umoja na wingi wa baadhi ya vitu.
Kituo hicho chenye jumla ya wasichana 54 kilianzisha mwaka 1990 kinatoa mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu ya Sekondari na msingi kwa wale ambao walikatisha masomo yao, ufundi wa kujitegemea, mapishi, stadi za maisha, utengenezaji wa nywele, ushonaji wa nguo na mafunzo  ya kiroho.
Mama Kikwete ameambatana na mumewe Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Singapore kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Mama Salma Kikwete atembelea kituo cha kurekebisha tabia kwa Wanawake na Wasichana watukutu cha Pertapis nchini Singapore.

Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo Mama Salma Kikwete akipokea ua kutoka kwa msichana anayetunzwa katika kituo cha watoto wa kike watukutu cha Pertapis kilichoko Singapore wakati alipokitembelea kituo hicho tarehe 6.6.2013. Mama Salma yupo nchini Singapore akiambatana na Rais Kikwete katika ziara ya kikazi ya siku mbili nchini humo. Kulia ni Mkuu wa kituo hicho Mama Sahnim Sokaimi.


Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwa katika mazungumzo rasmi na uongozi wa kituo cha kuwatunza wasichana na wanawake watukutu cha Pertapis kilichoko nchini Singapore.


Mwenyekiti wa WAMA na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisisitiza jambo wakati wa kikao cha pamoja kati yake na uongozi wa kituo cha kuwarekebisha tabia wanawake na wasichana cha Pertapis kilichoko huko Singapore wakati alipokitembelea tarehe 6.6.2013. Kushoto kwa Mama Salma ni Mama Badriya Kiondo, Afisa kutoka ubalozi wa Tanzania nchini India. 


Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoa somo kwa wasichana watukutu wanaotunzwa kwenye kituo cha kurekebisha tabia zao cha Pertapis kilichoko jijini Singapore wakati alipokitembelea tarehe 6.6.2013.


Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akizungumza na Mama Sahnim Sokaimi, Mkuu wa kituo cha kurekebisha tabia za wanawake na wasichana watukutu cha Pertapis kilichoko nchini Singapore mara baada ya kukitembelea tarehe 6.6.2013.

(Picha zote na John Lukuwi)