Saturday, 25 April 2015

Elimu ya uongozi bora yatolewa kwa viongozi wa vikundi vya vijana Kata ya Selela

Mhamasishaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa katikati akizungumza na Vijana wa Kata ya Selela (hawapo pichani) wakati wa semina ya Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana jana katika Kata ya Selela Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha. Kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele na kulia ni Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara hiyo Bi. Amina Sanga

Vijana wa Kata ya Selela wakisikiliza kwa makini mada zilizokua zikitolewa wakati wa semina ya Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana jana katika Kata ya Selela Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.

Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Bi. Mesha Singoyo akifafanua jambo kwenye semina ya vijana wa Kata ya Selela kuhusu Ujasiriamali, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana iliyofanyika jana katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha

Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga (kulia) akizungumza na wanakikundi cha Naisho wanaomiliki mradi wa kunenepesha ng’ombe na kuziuza wakati wa kutembelea miradi ya vijana wa Kata ya Selela Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha. Wapili kushoto ni mhamasishaji kutoka Wizara hiyo Bibi. Ester Riwa na wanne kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele.

Baadhi ya ng’ombe zinazomilikiwa na vijana wa Naisho Group zikiwa machungani katika kata ya Selela Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.

Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele (wapili kulia) akifafanua jambo walipotembelea mradi wa kikundi cha Songambele kinachojishughulisha na kilimo katika Kata ya Selela Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha. Kulia ni mhamasishaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi. Ester Riwa.

Moja ya shamba la mahindi linalomilikiwa na kikundi cha Songambele katika kata ya Selela Halmashauri ya Wilaya ya Mondili Mkoani Arusha.

Picha/Habari na: Genofeva Matemu 

Viongozi wa vikundi vya vijana wametakiwa kuwa waadilifu na wenye kutoa haki sawa katika vikundi vyao bila ya kuhusisha masuala ya udini, ukabila au uanachama wa chama fulani kwani kwa kufanya hivyo watafikia malengo waliyojiwekea katika vikundi vyao.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele wakati wa semina ya vijana wa Kata wa Selela kuhusu Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana jana katika kata Selela Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.

Bw. Masele amesema kuwa kiongozi ndie chachu ya maendeleo ya kikundi kama atakua kiongozi bora na mwenye maadili mema, anayejitolea na mwenye kuongoza vijana wenzake kwa haki bila kutumia mabavu ama kuwa na jazba.

“Viongozi wa vikundi vya vijana acheni kutumia fursa mlizonazo kwa maslahi yenu binafsi mnapaswa kuonyesha njia iliyo sahihi kwa wanachama wa vikundi huku mkiwatia moyo wanakikundi kuongeza jitihada kufikia malengo mliyojiwekea bila kujali vikwazo vidogovidogo vinavyoweza kutokea ndani ya vikundi vyenu” amesema Bw. Masele.

Aidha Diwani wa Kata ya Selela Mhe. Yese Runda ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo kuwafikika vijana wa Selela na kuwapatia elimu ya ujasiriamali kwani vijana wa kata hiyo wanamuamko mkubwa wa kuleta maendeleo katika kata yao kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

“Nawapongeza vijana wa Kata ya Selela hasa viongozi wa vikundi vya vijana kwa kuhakikisha kuwa mila na desturi za kabila la kimasai haziingiliani na maendeleo yaliyopo katika jamii kwani wakati wa kufanya kazi za maendeleo mila zinawekwa pembeni ili kuleta ubora na ufanisi wa maendeleo yaliyo imara katika kata yetu” amesema Mhe. Runda.

Nae kijana Meja Nailenya amewataka vijana wenzake nchini kuachana na maneno yasiyokuwa na msingi bali watumie muda wao vizuri kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili waweze kusimama imara na kuacha kuitegemea serikali kwa kila jambo.

Nailenya amesema kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa huduma muhimu zinaifikia jamii kama vile huduma ya afya na huduma ya maji salama hivyo kuiomba serikali kuendelea kufikisha huduma hizo muhimu kila inapopata nafasi hasa huduma ya barabara ambayo babo ni changamoto katika Kata ya Selela.